IQNA

Waislamu India

Watu watano wauawa India katika maandamano baada ya kubomolewa Misikiti

17:53 - February 09, 2024
Habari ID: 3478323
IQNA - Takriban watu watano wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa wakati wa maandamano yaliyotokana na ubomoaji wa msikiti na shule wa Kiislamu nchini India, ikiwa ni tukio la hivi punde zaidi katika msururu wa ubomoaji unaolenga majengo ya Waislamu.

Mamlaka ya manispaa katika mji wa Haldwani katika jimbo la kaskazini la Uttarakhand walivamia majengo hayo siku ya Alhamisi, wakisema kuwa yamejengwa bila ruhusa.

Polisi walisema Waislamu waliokuwa na hasira walichoma magari na kuwarushia mawe katika maandamano yaliyofuata. Katika ghasia hizo polisi walitumia risasi na kuwaua waandamanaji.

Wakaazi walisema majengo ya msikiti na shule katika eneo la Banphoolpur la Haldwani yalijengwa takriban miongo miwili kwa vibali na hiyo ilikuwa si haki kubomolewa.

Afisa wa juu wa polisi huko Uttarakhand siku ya Ijumaa aliambia gazeti la The Indian Express kuwa watu watano waliuawa katika maandamano hayo, lakini hakuwatambua.

Mamlaka katika eneo la Haldwani imetoa maagizo ya kufyatua risasi kwa atakayekiuka  amri ya kutotoka nje. Aidha watawala wa eneo hilo wamesimamisha huduma za mtandao sambamba na kufunga shule na kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa.

Sumit Hridayesh, mbunge wa jimbo kutoka chama cha upinzani cha Indian National Congress ambaye anawakilisha Haldwani, alisema ghasia hizo zilitokana na "hatua za hamaki" za utawala. Alisema wenyeji wa eneo hilo wakiwemo viongozi wa Kiislamu walipaswa kupewa taarifa kabla ya ubomoaji huo kutekelezwa.

Makundi ya itikadi kali ya Kihindu yamejizatiti katika kampeni yao dhidi ya Waislamu na taasisi zao za kidini tangu Waziri Mkuu Narendra Modi aingie madarakani muongo mmoja uliopita.

Mwezi uliopita, Modi alifungua hekalu la Kihindu katika mji wa kaskazini wa Ayodhya. Hekali hilo limejengwa kwenye uwanja wa msikiti wa kale wa zamaa za Mughal ambao uliharibiwa na Wahindu wenye misimamo mikali mwaka 1992.

Waislamu wanalaumu serikali za mikoa  zinazodhibitiwa na Chama cha Bhartiya Janata (BJP) cha Modi kwa kutumia tingatinga kubomoa nyumba na biashara za Waislamu katika kile kinachoonekana ni kampeni ya wazi ya chuki.

Katika ripoti mbili zilizochapishwa kwa pamoja wiki hii, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliandika ubomoaji wa angalau mali 128 za Waislamu kuanzia Aprili hadi Juni 2022, umesababisha watu wasiopungua 617 kukosa makazi au kukosa riziki.

Mashirika ya haki za binadamu pia yamemshutumu Modi kwa kupuuza na wakati mwingine kuwezesha matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu, ambao ni asilimia 14 ya watu bilioni 1.4 wa India.

3487131

captcha