IQNA

Mtukio ya hivi karibuni Afghanistan

Wamarekani wengi wanaamini nchi yao imeshindwa na kufeli Afghanistan

21:57 - September 03, 2021
Habari ID: 3474253
TEHRAN (IQNA)- Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Marekani yanaonesha kuwa, asilimia 69 ya watu wa nchi hiyo wanaamini kuwa nchi yao imefeli na kushindwa kutimiza malengo yake huko Afganistan.

Tovuti ya The Hill imeandika kuwa, uchunguzi wa maoni wa kituo cha utafiti cha PEW uliofanyika wiki ya mwisho ya kuondoka wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan unaonesha kuwa, asilia 54 ya Wamarekani wanaamini kuwa, uamuzi wa serikali ya Washington wa kuondoa jeshi la nchi hiyo huko Afghanistan ulikuwa sahihi.

Ripoti hiyo inasema asilimia 69 ya Wamarekani walioshiriki katika uchunguzi wa maoni wanasema Marekani imeshindwa kufikia malengo yake huko Afghanistan. 

Awali matokeo ya uchunguzi wa maoni wa televisheni ya ABC News na taasisi ya Ipsos yalionesha kuwa siku za tarehe 27 na 28 za mwezi uliopita wa Agosti na baada ya mlipuko mkubwa uliotokea uwanja wa ndege wa Kabul vimeonesha kuwa, zaidi ya nusu ya Wamarekani yaani asilimia 56 wanasema uwepo wa majeshi ya Marekani nchini ya Afghanistan haukuwa na taathira katika kupunguza ugaidi.

Hivi karibuni pia kituo cha American Enterprise kiliripoti kuwa gharama za kuwepo majeshi ya Marekani huko Afghanistan zinakadiriwa kufikia trilioni kadhaa dola.

Baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001 katika miji ya New York na Washington, Marekani iliivamia na kuishambulia nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuiondoa madarakani serikali ya kundi la Taliban ambalo inalituhumu kuwa lilishirikiana na al Qaida katika mashambulizi ya Septemba 11. 

Takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, madawa ya kulevya, uharibifu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Katika kipindi hicho wanajeshi 2,448 wa Marekani wameuawa wakiwa vitani, na vilevile wanajeshi 1144 wa shirika la NATO wameuawa katika vita hivyo. 

Afrika Kusini yakataa wakimbizi Waafghani

Afrika Kusini imesema haiko katika nafasi ya kupokea wakimbizi wa Afghanistan ambao wamekimbia nchi yao kwenda nchi jirani ya Pakistan.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano (DIRCO) ilisema katika taarifa kuwa, "Serikali ya Afrika Kusini imepokea maombi ya kupokea wakimbizi kadhaa wa Afghanistan ambao wametafuta hifadhi nchini Pakistan.”

Idara hiyo imesema kuwa nchi hiyo imeombwa kuwapa makao wakimbizi hao wanaposafiri wakiwa njiani kuelekea maeneo yao ya mwisho.

"Kwa bahati mbaya serikali ya Afrika Kusini haina uwezo wa kukubali ombi kama hilo," ilisema.

DIRCO ilisema Afrika Kusini tayari ni mwenyeji wa idadi kubwa ya wakimbizi na inashughulika mahitaji yao.

Afrika Kusini ilisema wakimbizi wengi ambao tayari wanahifadhi wananufaika na mipango yake ya msaada wa kijamii, pamoja na mipango ya bure ya afya ya matibabu inayotolewa na nchi hiyo.

"Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, usalama wa wakimbizi unashughulikiwa kwa njia bora zaidi kwa kubaki katika nchi ya kwanza waliyowasili, na kwa kesi hii ni, Pakistan ,  wakisubiri maeneo yao ya mwisho," ilisema taarifa hiyo. Hivi karibuni pia Namibua ilitangaza kukataa ombi la Marekani la kuwapokea wakimbizi hao wa Afghanistan.

Uganda na Rwanda ni nchi za Afrika ambazo zimekubali kutoa hifadhi ya muda kwa wakimbizi wa Afghanistan wanaosubiri makazi mapya Marekani na mataifa mengine tajiri ya Magharibi. Aghalabu ya wakimbizi hao ni wale ambao walikuwa wakifanya kazi na muungano wa kijeshi wa NATO unaaongoza na Marekani na sasa wanasema maisha yao yako hatarini iwapo watabakia Afghanistan wakati huu ambapo serikali imechukuliwa na kundi la Taliban.

Kauli ya Russia

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan kuna maana ya mwisho wa kulazimisha demokrasia kwa kutumia nguvu za kijeshi.

Sergey Lavrov amesema sasa hapana shaka kuwa nchi za Magharibi zitatumia njia zisizo za kijeshi kwa ajili ya kudumisha sera zao za kueneza "demokrasia" na kuzitwisha nchi nyingine thamani na mitindo yao ya kimaisha. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rusia pia amesema Moscow haina nia ya kuwa mpatanishi baina ya makundi ya Waafghani na inatarajia kuwa mivutano iliyopo baina ya makundi hayo itatatuliwa kupitia njia ya mazungumzo. 

Awali na kufuatia kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan baada ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 20 na vilevile milipuko na machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo siku za karibuni, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan kumesababisha maafa matupu. 

Majeshi ya Marekani na waitifaki wake wa Ulaya yameondoka Afghanistan kwa madhila na fedheha baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 20. 

3994791

captcha