IQNA

Matukio ya Afghanistan

Kundi la Taliban latangaza kumteua rais wa Afghanistan

18:57 - September 06, 2021
Habari ID: 3474265
TEHRAN (IQNA)- Imearifiwa kuwa, kundi la Taliban la Afghanistan limempendekeza Mullah Hassan Akhund kuwa rais wa baadaye wa nchi hiyo.

Kiongozi wa kundi la Taliban, Hibatullah Akhundzada amependekeza Muhallah Hassan Akhund kuwa Rais, au Waziri Mkuu au Msimamizi mpya wa serikali ya Afghanistan na Mulla Baradar Akhund na Mulla Abdus Salaam kuwa manaibu wake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi la Taliban limeshamaliza mipango yote ya kutangaza serikali mpya. Serikali hiyo ilikuwa itangazwe rasmi jana Jumatatu lakini kutokana na sababu mbalimbali, zoezi hilo limeakhirishwa. Baadhi ya viongozi wa Taliban wamesema kuwa, kuna uwezekano serikali mpya ya Afghanistan ikatangazwa rasmi kesho Jumatano au ikaakhirishwa tena kwa siku kadhaa.

Hivi sasa Mullah Hassan Akhund ni mkuu wa chombo chenye nguvu zaidi za kuchukua maamuzi ndani ya kundi la Taliban yaani Baraza la Uongozi na ni mmoja wa waanzilishi wa kundi lenye silaha ndani ya Taliban. Ana uzoefu wa kuongoza Baraza la Uongozi la Taliban kwa muda wa miaka 20.

Ikumbukwe kuwa, hadi hivi sasa kundi la Taliban halijapata uungaji mkono wa Waafghani wote. Siku chache zilizopita, Ahmad Masoud, Kiongozi wa Waafghanistan wanaolipinga kundi la Taliban alitoa mwito wa kuendelezwa mapambano dhidi ya kundi hilo. Ahmad Masoud, ambaye ni mwana wa Ahmad Shah Masoud, shujaa wa taifa wa Afghanistan alisema kwamba: "Hatutaacha katu kupambana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, uhuru na uadilifu."

Hayo yanajiri wakati ambao kundi la Taliban limetangaza kuuteka mkoa wa Panjshir ambao ulikuwa mikononi mwa wapiganaji wa Ahmad Masoud madai ambayo yamepingwa na wakazi wa eneo hilo.

3995528/

Kishikizo: taliban afghanistan
captcha