IQNA

Ta'azia

Msiba Mkubwa kwa Taifa': Afghanistan yamuomboleza Qari Mkuu Barakatullah Saleem

16:00 - January 28, 2024
Habari ID: 3478263
IQNA - Qari Barakatullah Saleem, msomaji na mwanazuoni mashuhuri wa Qur'ani Tukufu wa Afghanistan, alifariki siku ya Jumamosi mjini Kabul baada ya kuugua, familia yake ilithibitisha.

Kifo cha Saleem kimeombolezwa na Waafghanistan wengi na Waislamu kote ulimwenguni, ambao wametuma taarifa kupitia mitandao ya kijamii wakimkumbuka kwa kazi zake zenye thamani. Wanafunzi wake na wasomi wenzake wamesifu kwa huduma na juhudi zake kwa ajili ya Qur'ani Tukufu na taifa la Afghanistan.

"Mwalimu wangu, Qari Barkatullah Saleem, amewatumikia wananchi wenzake kwa miaka mingi na amefanya juhudi bila kuchoka kwa njia hii," alisema Naqib Rahman, mmoja wa wanafunzi wake .

"Kifo cha Qari Barkatullah Saleem ni hasara kubwa kwa taifa la Afghanistan," alisema Amanullah Ahmadi, mwanazuoni wa kidini, Tolo News iliripoti Jumamosi.

Sheikh Saleem, aliyezaliwa mwaka 1950 katika jimbo la Nangarhar, mashariki mwa Afghanistan, alipoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miezi 14. Licha ya changamoto hii, alionyesha kipawa cha ajabu na kujitolea katika qiraa ya Qur'ani Tukufu, akiongozwa na baba yake, Molavi Ghalajan, mwanazuoni aliyeheshimika wa wakati wake. Saleem alihifadhi Qur'ani yote akiwa na umri wa miaka tisa na alijifunza Tajweed kutoka kwa baba yake. Kisha alihudhuria shule ya Qur'ani ya mahali hapo, ambapo alifaulu katika kusoma na kufasiri.

Mnamo 1964, Saleem alisafiri kwenda Misri kwa msaada wa kifedha wa mfanyabiashara ambaye alifadhili wanafunzi kujifunza Qur'ani Tukufu. Huko, alisoma chini ya maqari mashuhuri kama vile Sheikh Mahmoud Khalil al-Hussary na Abul Ainain Shuaisha. Alisoma Misri kwa muda wa miaka sita huko Misri, ambapo alijifunza mitindo kumi ya qiraa, jambo ambalo ni mafanikio adimu.

Aliporejea Afghanistan, alibadilisha mbinu za kuhifadhi Qur'ani na kuwa mtu mashuhuri katika duru za kidini kupitia kazi yake na Radio Kabul. Pia alianzisha chama cha maqari wa Afghanistan katika miaka ya 1990 na kubakia kiongozi  hadi kifo chake.

Sheikh Saleem alikuwa mmoja wa walimu wa Qur'ani wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Afghanistan, akiwa ametoa mafunzo kwa wahifadhi zaidi ya 800 katika kipindi cha miaka 52 iliyopita. Alikaa Kabul katika mazingira yote ya kisiasa yaliyokuwa yakibadilika, akijiweka mbali na siasa na kulenga kuitumikia Qur'ani Tukufu.

Alielezea wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa maqari wenye sifa nchini Afghanistan, akisema hilo linatokana na kutofahamu kanuni za Tajweed na mitindo ya qiraa. Alirekodi qiraa ya Qur'ani  katika mitindo kadhaa kwa ajili ya televisheni na aliandika vitabu 13, ambavyo baadhi hutumika kama vitabu katika mitala ya shule na vyuo vikuu.

3486981

Habari zinazohusiana
captcha