IQNA

Misaada kwa Syria

Shehena ya tano ya misaada ya kibinadamu ya Iran yawafikia waathirika wa mitetemeko ya ardhi Syria

18:52 - February 09, 2023
Habari ID: 3476537
TEHRAN (IQNA)- Shehena ya tano ya misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa watu waliokumbwa na mitetemeko ya ardhi nchini Syria iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus mapema leo Alhamisi.

Aidha shehena ya nne pia jana Jumatano ilifika katika uwanja wa kimataifa wa Aleppo.

Salman Nawab Nouri, Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Aleppo amesema kuhusiana na misaada ya jana kwamba: Shehena ya nne ya misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa watu wa Syria, iliyowasili katika uwanja wa ndege wa Aleppo, inajumuisha  mahema, tende, mchele, samaki za makopo (tuna) pasta na kadhalika.

Ndege tatu zilizokuwa zimebeba misaada kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa watu walioathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea hivi karibuni nchini Syria, zilikuwa tayari zimewasili nchini humo.

Ndege ya kwanza ilishusha mizigo yake katika uwanja wa ndege wa Damascus, ndege ya pili ilitua katika uwanja wa ndege wa Aleppo, na ndege ya tatu ilitua Latakia na kushusha misaada ya kibinadamu kwa ajili ya waathiriwa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa kinara kati ya nchi marafiki wa Syria katika kutuma misaada ya kibinadamu na kuvunja vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi dhidi ya wananchi wa Syria.

Tetemeko la kwanza la  ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari. Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka.Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.

Ikiwa yameshapita masaa 72 tangu kutokea kwa janga hilo, wataalamu wa maafa wameonesha wasiwasi wao wa kuweza kuokoa maisha zaidi. Mamlaka zimefahamisha kuwa watu karibu 20,000 wamefariki katika nchi hizo mbili huku Uturuki ikiwa imepoteza idadi kubwa zaidi ya watu ambapo Alhamisi Rais Reccep Tayyip Erdogan alitangaza idadi ya walipoteza maisha nchini humo ilikuwa imefika  16,546.

IRNA

 

captcha