IQNA

Watetezi wa Palestina

Maandamano makubwa yafanyika Ulaya kuunga mkono Palestina, kulaani Israel

22:17 - October 29, 2023
Habari ID: 3477810
TEHRAN (IQNA) -Makumi kwa maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina waliandamana nchini Uingereza Jumamosi wakitaka kusitishwa kwa mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Mbali na Uingereza, maandamano kama hayo yamefanyika pia Ufaransa na Uswisi.

Maandamano hayo ya waungaji mkono wa Palestina yamejiri huku utawala dhalimu wa Israel ukijaribu kutumia mashambulizi makali ya anga kuvipa himaya vikosi vyake vya nchi kavu ili kushadidisha vita dhidi ya Ghaza, ambapo Umoja wa Mataifa umeonya maelfu ya raia zaidi wanaweza kufa.
Utawala katili wa Israel ulianzisha mashambulizi yake ya ya kinyama dhidi ya eneo lililozingirwa la Ghaza mnamo Okotba 7  baada ya makundi ya muqawama au wapigania ukombozi wa Palestina wenye makao yao Ghaza kuanzisha Operesheni Kimbunga au Tufani ya al-Aqsa kwa lengo la kukabiliana na jinai za utawala huo.
Wizara ya afya ya Ghaza inasema mashambulizi ya Israel tangu wakati huo yameua zaidi ya Wapalestina 8,000, ambapo zaidi ya 3,000 kati yao wakiwa watoto.
Hii ni wikendi ya tatu mfululizo ambapo wakazi wa London waliandaa mjumuiko mkubwa wa kuwaunga mkono Wapalestina.
Waandamanaji hao walikusanyika katikati mwa Mto Thames saa sita mchana, kabla ya kuelekea katika bunge la Uingereza huko Westminster.
Takriban watu 100,000 walijiunga na "Matembezi kwa Ajili ya  Palestina" huko London kulingana na vyombo vya habari vya Uingereza, ambavyo pia viliripoti kuwa maafisa wa polisi walijaribu kuvuruga maandamano hayo ya amani.
Maelfu ya waandamanaji pia walishiriki katika maandamano kote Ufaransa siku ya Jumamosi. Waandamanaji walijumuika mjini Paris, na kukaidi marufuku ya kuandamana  kwa ajili ya kupinga jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina. Kikosi kikubwa cha polisi kilikabiliana na waandamanaji katikati mwa mji mkuu.

Miongoni mwa waandamanaji walikuwa viongozi waliochaguliwa, akiwemo mbunge wa Kijani na mbunge wa mrengo wa kushoto.
Elsa Toure, naibu meya wa Corbeil-Essonnes, kusini mwa Paris akizungumza katika maandamano hayo alisema: "(Haja ya) kusitishwa kwa mapigano ni ya dharura." Aidha alisema kuna udharura kwa Israel  kukomesha kuua wanawake, watoto na wanaume.
Waandamanaji pia waliingia barabarani katika miji mingine ya Ufaransa.

Waandalizi walisema watu 4,000 waliandamana katika mji wa kusini wa Marseille. Katika nchi jirani ya Uswisi, waandaaji walisema waandamanaji 7,000 walikusanyika Zurich. Maandamano makubwa pia yalifanyika katika miji ya Lausanne, Geneva na Bern.

Siku ya Ijumaa pia maandamano yalifanyika katika maeneo mbali mbali ya dunia kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina. Barani Afrika maandamano yalifanyika Mauritania, Tunisia na Nigeria. Maandamano kama hayo ya kulaani utawala haramu wa Israel yamefanyika siku za hivi karibuni katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Kenya, Nigeria na Morocco.

3485775

captcha