IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu /21

Sheikh Abd al-Hamid Kishk aliandika Tafsiri ya Qur’ani kwa lugha sahali

23:09 - February 27, 2023
Habari ID: 3476635
TEHRAN (IQNA) – Sheikh Abd al-Hamid Kishk alikuwa mhubiri wa Misri, mfasiri wa Qur'ani, msomi wa Uislamu, mwanaharakati, na mwandishi. Alikuwa miongoni mwa wahubiri mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu na ameacha turathi ya hotuba zaidi ya 2,000.

Abd al-Hamid bin Abd al-Aziz Kishk alizaliwa Machi 1933 huko Shubra Khit, mji ulioko katika Jimbo la Beheira nchini Misri. Alikwenda Maktab (shule ya Kiislamu) akiwa na umri mdogo na aliweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kwa moyo kabla ya kumi.

Kisha akaenda katika kituo cha kidini huko Alexandria na alikuwa mwanafunzi bora katika mtihani wa mwisho wa shule za upili za Al-Azhar kote Misri. Aliingia Chuo Kikuu cha Al-Azhar na huko, pia, kulikuwa na wanafunzi wa juu.

Sheikh Kishk aliidhinishwa kuwa mwalimu katika kitivo cha misingi ya kidini cha Chuo Kikuu cha Al-Azhar mwaka wa 1957. Hata hivyo, alipenda zaidi kuhubiri na ndiyo sababu aliacha ualimu katika chuo kikuu hicho.

Alipoteza uwezo wake wa kuona kwa macho akiwa na umri wa miaka 13 na kisha jicho lingine akiwa na miaka 17. Alikuwa akisoma shairi maarufu la Ibn Abbas linalosema “Mungu aliyaondoa macho yangu lakini akaipa nuru  nafsi yangu na mawazo yangu”.

Aliandika vitabu 108 vya elimu ya Kiislamu na  fikra  za Qur’anii Tukufu. Katika vitabu hivi, anatumia lugha rahisi kueleza kuhusu Uislamu na madhumuni ya aya za  Qur’ani Tukufu kwa lugha inayoeleweka miongoni mwa watu wa kawaida.

Tafsiri ya Qur’ani Tukufu iliyoandikwa na Sheikh Abd al-Hamid Kishk inajulikana kama Fi Rihabi-t-Tafsir na ina juzuu kumi ambamo ametumia lugha rahisi kuangazia mwongozo wa Qur’an Tukufu katika maeneo tofauti.

Mbinu ya lugha na tafsiri iliyotumika katika tafsiri hii inawarahisishia watu wa kawaida wasio na elimu ya Qur'ani na wasio na weledi kilugha, kielimu na kifiqhi kufaidika nayo.

Katika tafsiri hii, Sheikh Kishk anataja kwanza kila Aya, kisha anaeleza kuhusu maneno yake mushimu  na kisha anazungumzia maana na madhumuni ya Aya. Kulingana na somo, yeye hutumia nyanja zingine za maarifa kama vile fasihi, sayansi ya siasa, dawa, n.k ili kuwasilisha maana bora. Kisha anaashiria maswali na mashaka juu ya dhana anayozungumzia na hatimaye anatoa maelezo sahali.

Katika khutba zake, Sheikh Kiskh alisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za maadili ya Kiislamu na Taqwa (kumcha Mungu), akizingatia nukta hii kuwa ni sababu ya ukuaji wa jamii.

Siku ya Ijumaa, Desemba 6, 1996, alipokuwa akijiandaa kwenda msikitini kusali Sala  ya Ijumaa, Sheikh Kishk alifariki dunia katikati ya Sala ya Nawafil.

captcha