OCHA ilisema katika ripoti mpya kwamba "vizuizi vya muda mrefu vya watu na bidhaa kutoka Gaza vimedhoofisha hali ya maisha ya zaidi ya wakazi milioni mbili wa Palestina."
"Israel inaendelea kupunguza upatikanaji wa riziki, huduma muhimu, na makazi, kuvuruga maisha ya familia, na kudhoofisha matumaini ya watu ya mustakabali salama na ustawi," imesema ripoti hiyo ya OCHA ambayo imeongeza kuwa hali hii mbaya pia imechangiwa na vizuizi vilivyowekwa na mamlaka ya Misri huko Rafah.
Tangu mwaka 2007, utawala katili wa Israel uliweka mzingiro wake kinyume cha sheria kwenye Ukanda wa Gaza, wenye makazi ya zaidi ya watu milioni 2.3, baada ya harakati ya Kiislamu ya Hamas kushinda katika uchaguzi huru wa wabunge mwaka 2006.
Aidha utawala haramu wa Israel umeanzisha vita vikubwa vitano vya kijeshi dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kuua na kujeruhi maelfu ya raia wa eneo hilo na kuharibu sehemu kubwa ya vituo vya huduma muhimu kwa raia kama vile shule, hospitali, misikiti na nyumba za raia.
Tangu kuwekwa kwa kizuizi hicho mwaka wa 2007, mamlaka za Israel zilizuia kuingia kwa bidhaa muhimu za Gaza kwa kisingizio kwamba zitakuwa na matumizi ya kiraia na kijeshi kama vile vifaa vya ujenzi, vifaa vya matibabu, na baadhi ya bidhaa za kilimo.
Mzingiro haramu wa utawala dhalimu wa Israel umepelekea Ukanda wa Gaza utajwe kuwa gereza kubwa zaidi la wazi kuwahi kushuhudiwa duniani huku wakazi wake wakiendelea kutaabika na matatizo mbalimbali ikiwa ni natija ya mzingiro huo wa kiuchumi.
3482300