IQNA

Waislamu India

Pesa kuchangishwa kwa ajili ya Ujenzi wa Msikiti huko Ayodhya nchini India

13:38 - August 21, 2022
Habari ID: 3475657
TEHRAN (IQNA) - Mpango unatayarishwa wa kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa msikiti katika kijiji cha Dhannipur cha Ayodhya katika jimbo la Uttar Pradesh nchini India.

Itajengwa kwenye ardhi ya ekari tano waliyopewa Waislamu kwa maelekezo ya Mahakama ya Juu ya India.

Novemba 2019, Mahakama Kuu ya India imewapokonya Waislamu ardhi ya Msikiti wa kihistoria wa Babri na kuwakabidhi Mabiniani (Wahindu) eneo hilo ili wajenge hekalu lao.

Majaji walidai kuwa msikiti huo uliokuwa umedumu kwa muda wa miaka 460, haukujengwa katika eneo tupu la ardhi, bali ulichukua nafasi ya hekalu lililokuwepo mahali hapo kabla yake.

Badala yake wamesema, Waislamu watapatiwa eneo jengine la ardhi yenye ukubwa wa ekari tano kwa ajili ya kujenga msikiti mwingine.

Taasisi ya Indo Islamic Cultural Foundation (IICF) ambayo imeanzishwa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo itajenga msikiti pamoja na hospitali, maktaba, jiko la jamii na taasisi ya utafiti katika ardhi hiyo.

Katibu wa Foundation Athar Hussain amesema  kwamba timu ya watu watano wakiongozwa na rais wake Zufar Farooqui walitembelea Farrukhabad mnamo Agosti 12 na kwa mara ya kwanza walitoa ombi la michango kwa ajili ya ujenzi wa msikiti na vifaa vingine vya umma huko Ayodhya.

Inatarajiwa kuwa ndani ya mwezi mmoja ramani ya msikiti huo na majengo mengine yatapatikana kutoka kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Ayodhya. Mara tu ramani itakapopokelewa, kazi ya ujenzi itaanza.

Mahakama Kuu ya India mnamo Novemba 9, 2019 iliamuru kwamba ekari tano zitolewe mahali maarufu huko Ayodhya kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huku ikiruhusu ujenzi wa hekalu la Kihindu la Ram huko Ayodhya.

Miaka 30 iliyopita magenge ya Wahindu wenye misimamo mikali walibomoa msikiti wa kihistoria wa Masjid Babri mjini Faizabad, na kusababisha wimbi la umwagaji damu baina ya Waislamu na Wahindu ambapo maelfu ya watu waliuawa. Katika hujuma hiyo Waislamu zaidi ya 2,000 waliuawa kinyama.

Ubomoaji huo pia ulikuza itikadi potovu ya Hindutva  ambayo inasisitiza Uhindu ni itikadi bora zaidi. Tukio la kubomolewa Msikiti wa Babari kimsingi  liliandaa njia ya kuinuka kwa Narendra Modi madarakani mnamo 2014.

3480177

captcha