IQNA

Waislamu Afrika

Wakimbizi Waislamu DRC wakumbwa na matatizo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani

16:30 - March 31, 2023
Habari ID: 3476791
TEHRAN (IQNA)- Idadi kubwa ya Waislamu waliyoyakimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na ghasia na machafuko, wanataabika na kuteseka katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika mji wa Munigi uliopo yapata kilomita kumi kutoka mstari wa vita na mapambano baina ya makundi ya waasi na jeshi la serikali hali ni mbaya kwani wakimbizi hao Waislamu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na chakula.

Waislamu hao wamejenga msikiti wao mdogo kwa kutumia mbao na makaratasi ya nailoni na hivyo kutumika kwa ajili ya ibada. Baadhi ya wakimbizi hao Waislamu wanasema, wanafunga kwa shida kutokana na kutopata futari na daku ya kutosha huku changamoto kuu ikiwa ni maji.

Ali Assan Mukamba Imamu wa Munigi anasema: Hapa hatuna maji, kabla ya kuswali mara nyingi tunalazimika kutayamamu (kutia udhu kwa kutumia udongo).

Mmoja wa wakimbizi hao Waislamu ambaye ni mtu mzima kiumri anasema, hivi sasa alhamdulihali hali imeboreka kwani kwa hisani ya baadhi ya wafadhili tunapata cha kutia kinywani wakati wa kufuturu.

Mussa Ahmad mmoja wa viongozi wa jamii ya Waislamu katika jimbo la Kivu Kaskazini amewaambia waandishi wa habari kwamba: Wakimbizi hao wanashikamana na ibada ya funga ya Ramadhani kwa sababu ni jambo la wajibu lililofaradhishwa na Mwenyezi Mungu hata katika mazingira ya kuweko vita. Tunafanya hima na juhudi za hapa na pale kutafuta wafadhili wa kuwasaidia ili kuwapunguzia ugumu wa Saumu wa kuwa na uhaba wa futari na daku.

Africanews

 

captcha