Kamati ya Dharura yenye mfungamano na harakati ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala ghasibu wa Israel imetangaza kuwa, Intafadha ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel haitosita mpaka pale matakwa ya mateka na wafungwa wa Kipalestina yatakapotekelezwa kikamilifu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa kuzingatia hatua zisizo za kibinadamu zinazotekelezwa na utawala vamizi wa Israel, kumeibuka mgomo mkubwa wa kususia chakula ukiwashirikisha wafungwa wote.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umesambaza kwa makusudi virusi vya corona katika jela ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa na utawala huo.
Hii ni katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni kitongoji cha Sheikh Jarrah katika eneo la Quds kimekumbwa na mashambulizi makubwa yanayofanywa walowezi na wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Makumi ya familia za Kipalestina zinazoishi katika kitongoji hicho ziko hatarini kuhamishwa kwa nguvu na utawala vamizi wa Kizayuni wa Israel.
Vitendo vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina ni mfano wa wazi wa ubaguzi wa apartheid kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uhalifu wa Ubaguzi.