Kwa mujibu wa taarifa katika tovuti ya youm7, Darul- Iftaa ya Misri imesambaza taarifa katika ukurasa wake rasmi wa Facebook na kuandika kuwa: “Tumeshauriana na kamati ya madaktari na kufikia natija kuwa, saumu haihusiki katika kuambukizwa corona na kwamba saumu husaidia kuimarisha zaidi kinga ya mwili katika kukabiliana na corona.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Iwapo saumu itakuwa na madhara kwa wagonjwa, madaktari na wauguzi ambao wako katika hatari ya kuambukizwa corona basi saumu kwao haijuzu.”
Aidha taarifa hiyo imesema saumu kwa walioambukizwa corona itategemea ushauri wa madaktari. “Iwapo daktari atashauri kuwa saumu kwa aliyeambukizwa itakuwa na madhara basi kutekeleza ushauri wa daktari ni wajibu kwa sababu kulinda afya kunapewa kipaumbele zaidi ya saumu,” imesema taarifa hiyo ya Darul Iftaa ya Msiri.
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umetabiriwa kuanza tarehe 25 Aprili na Waislamu maeneo mbali mbali ya dunia wanajitayarishwa kwa saumu huku janga la corona likiwe limeenea duniani.