Tume hiyo ya mahakama itaanzisha uchunguzi kuhusu mauaji
ya kutisha yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa mji wa
Zaria katija jimbo la Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Uchunguzi huo utaanza katika hali ambayo wiki iliyopita mashuhuda
waligundua kaburi la umati ambalo ndani yake ilizikwa miili 350 ya
Waislamu hao. Afisa mmoja wa tume hiyo ya uchunguzi amenukuliwa akisema
kuwa, baada ya umwagaji damu mkubwa uliofanywa na jeshi hilo, liliamua
kuizika miili ya wahanga katika kaburi hilo la umati. Amesema ushahidi
unaonyesha kwamba, kwa akali watu 350 waliuawa katika hujuma ya tarehe
12 mwezi Disemba mwaka jana mjini Zaria, kaskazini mwa nchi hiyo. Afisa
huyo ameweka wazi kwamba, siku moja baada ya mauaji hayo, mtu mmoja
asiyejulikana alimpigia simu na kumtaarifu juu ya kuwepo kaburi la umati
katika jimbo la Kaduna. Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Kiislamu
nchini humo, imetaka kuwekwa wazi jinai iliyofanywa na askari wa
serikali dhidi ya Waislamu katika tukio la mauaji ya Zaria. Aminu
Abubakar, mmoja wa wajumbe wa harakati hiyo hapo jana Ijumaa sanjari na
kulituhumu jeshi la nchi hiyo kwa kuhusika na mauaji dhidi ya Waislamu
wa nchi hiyo mjini Zaria, ametaka kufukuliwa miili ya wahanga wa mauaji
hayo kutoka kwenye kaburi hilo la umati mjini Kaduna. Hii ni katika hali
ambayo siku chache zilizopita, Harakati ya Kiislamu ilifanya maandamano
makubwa kwenda kwenye kaburi hilo. Wiki iliyopita pia Shirika la
Msamahama Duniani la Amnesty International lililituhumu jeshi la Nigeria
kwa kuwaua makusudi wafuasi wa harakati hiyo eneo lililotajwa ambalo
lipo umbali wa kilometa 80 jimboni Kaduna. Shirika hilo lilibainisha
kwamba aghlabu ya ushahidi wa jinai za Zaria uliharibiwa na jeshi hilo,
ikiwa ni pamoja na kuharibu kabisa kituo cha kidini cha harakati hiyo ya
Kiislamu na kadhalika makazi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi mkuu
wa harakati hiyo. Amnesty International iliongeza kuwa, madai ya jeshi
la nchi hiyo kwamba wafuasi wa harakati hiyo walikusudia kumuua kamanda
mkuu wa jeshi la Nigeria mjini Zaria, hayana msingi wowote na ni ya
kubuni tu. Kufuatia ripoti hiyo ya Shirika la Msamaha Duniani, Sani
Osman, msemaji wa jeshi hilo ameitaja ripoti hiyo kuwa ya pupa na isiyo
na itibari. Hata hivyo ukweli ni kwamba, kutolewa ripoti hiyo inaweza
kuwa sababu ya kuadhibiwa wahusika wa jinai hiyo na kulipwa fidia
familia za wahanga wake. Itakumbukwa kuwa, tarehe 14 mwezi Disemba mwaka
jana jeshi la Nigeria baada ya siku moja ya kufanya mauaji ya kutisha
dhidi ya Waislamu hao, liliizika kwa siri miili ya wahanga katika kaburi
moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Muhammadu
Mustafa, mjumbe wa harakati hiyo ya Kiislamu nchini Nigeria amesema
kuwa, serikali ya eneo katika jimbo la Kaduna, inadai kuwa watu
waliozikwa katika kaburi hilo la umati ni 347, katika hali ambayo idadi
halisi ya mauaji hayo inapindukia idadi hiyo. Wito wa kutaka wahusika wa
hujuma dhidi ya Husseiniyyah ya Waislamu hao waadhibiwe, unatolewa
katika hali ambayo maafisa wa Shirika la Msamaha Duniani Amnesty
International wamesema kuwa, hadi sasa idadi kubwa ya Waislamu bado
wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za jeshi la nchi hiyo huku
wengine wakiwa hawajulikani waliko. Wakati huo huo baadhi ya duru za
habari zimeripoti kwamba, jicho la kushoto la Sheikh Ibrahim Zakzaky,
Kiongozi wa harakati hiyo ya Kiislamu halioni huku mkono wake wa kushoto
pia ukielekea kupooza. Aidha hali ya kimwili ya mke wake nayo
inasemekana kuendelea kuwa mbaya siku hadi siku.
3493164