IQNA

Waislamu na Michezo

Nyota Muislamu Sadio Mane Ashinda Tuzo ya Mchezaji Bora Barani Afrika 2022

16:50 - July 24, 2022
Habari ID: 3475531
TEHRAN (IQNA)- Nyota Muislamu ambaye ni mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Soka ya Senegal Sadio Mane ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika.

Mane alikabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyoandaliwa jijini Rabat nchini Morocco na kuishinda tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo baada pia ya kuitwaa mwaka jana.

Mane alifunga penalti ya ushindi na kuisaidia Senegal kushinda kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza kwa kuwanyuka miamba wa AFCON Misri kupitia mikwaju ya penalti. “Nimefurahi sana kupokea tuzo hii mwaka huu,” Mane alisema akipokea tuzo hiyo.

Mshambuliaji huyo aliwapiku Edouard Mendy (kipa wa Chelsea na Senegal) na Mohamed Salah (mshambuliaji wa Liverpool na Misri) kutwaa tuzo hiyo. Mane ambaye ameiaga klabu ya Liverpool na kujiunga na Bayern Munich ya Ujerumani kwa mkataba wa miaka mitatu, pia aliisaidia Senegal kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia nchini Qatar baadaye mwaka huu.

Ilivyokuwa katika fainali ya AFCON, Mane alifunga penalti ya ushindi na Senegal kuwatandika Misri ili kufuzu kwa mashindano hayo ya ulimwengu. “Ninataka kuwashuruku watu wa Senegal na ninatoa tuzo hii kwa vijana wa taifa langu,” alisema Mane, ambaye alishinda vikombe viwili na Liverpool msimu jana. Tuzo ya mane ni moja tu kati ya tuzo tano zilizoshindwa na Senegal katika jumla ya vitengo saba vya tuzo za wanaume. Kocha wa Senegal Aliou Cisse alishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka, timu yake kutajwa timu yam waka ya wanaume, Pape Sarr kutajwa mchezaji mchanga bora zaidi huku Pape Ousmane Sakho (raia mwengine wa Senegal) akishinda tuzo ya bao bora zaidi alilofungia klabu yake ya Simba katika Champions League ya Afrika. Sadio Mane ni maarufu kama mchezaji ambaye hufunga katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani hata wakati anacheza mechi muhimu.

4072532

Kishikizo: sadio mane senegal
captcha