Al-Kadhimi amenukuliwa akisema: "Mamlaka ya kitaifa ya kujitawala ndicho kipaumbele changu cha kwanza."
Waziri Mkuu mteule wa Iraq amesisitiza kuwa, serikali haitaruhusu mtu yeyote yule amtusi raia yeyote wa Iraq kwa kumtuhumu kuwa ana mfungamano na maajinabi.
Aidha ameahidi kuwa baraza la mawaziri atakalounda litakuwa mstari wa mbele kutetea Wairaqi na kupambana na kirusi cha corona kinachosababisha maradhi ya COVID-19.
Kauli hiyo ya Mustafa al-Kadhimi imetolewa kufuatiwa hatua za kutia shaka zilizochukuliwa hivi karibuni na Marekani ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mapema mwezi huu Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilichukua hatua ya kuingiza nchini Iraq mifumo mipya ya makombora ya ulinzi wa anga ya Patriot bila kuipa taarifa serikali ya nchi hiyo, wakati miito inaendelea kutolewa kuwataka askari wa jeshi la Marekani waondoke nchini humo.
Kufuatia uamuzi wa Adnan al-Zurfi wa kughairi kuunda serikali mpya, na kutokana na maafikiano yaliyofikiwa kati ya makundi ya kisiasa ya kuunga mkono kuteuliwa Mustafa al-Kadhimi kuwa waziri mkuu mpya, siku ya Alkhamisi ya tarehe 9 Aprili Rais Barham Salih wa Iraq alimkabidhi rasmi al-Kadhimi jukumu la kuunda serikali mpya.