IQNA

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Waziri Mkuu wa Pakistan: Sote tukabiliane na chuki dhidi ya Uislamu

12:50 - September 25, 2021
Habari ID: 3474341
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema, kuna udharura wa kukabiliana na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu kieneo na kimataifa.

Imran Khan ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa njia ya mawasiliano ya video katika mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na akaeleza kwamba "uenezaji chuki dhidi ya Uislamu ni kitu kinachochukiza na inatupasa sote tukabiliane nacho."

Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa, mfumo tawala nchini India umeanzisha wimbi la uenezaji chuki, hofu na ukatiili dhidi ya Waislamu milioni mia mbili wa nchi hiyo.

Imran Khan amebainisha kuwa, kwa hatua yake hiyo, serikali ya India imekiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la Kashmir.

Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa, hatua inazochukua India katika eneo la Jamu na Kashmir ni uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Katika hotuba yake hiyo, Imran Khan amesema, sharti la kufikia suluhu na India ni serikali ya New Delhi kuhitimisha mzozo wa Jamu na Kashmir. 

Amesisitiza pia kwamba India inapaswa ikomeshe ukandamizaji, ukiukaji haki za binadamu na sera ya kubadilisha muundo wa idadi ya watu dhidi ya wananchi wa Kashmir.

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Waziri Mkuu wa Pakistan ameashiria pia matukio ya Afghanistan na akasema, kwa hivi sasa inapasa kuiunga mkono serikali ya muda ya Taliban ili kurejesha uthabiti katika nchi hiyo.

3475781

captcha