IQNA

Uhusiano wa kawaida wa Israel na nchi za Kiarabu haujawa na faida

11:41 - September 17, 2021
Habari ID: 3474304
TEHRAN (IQNA)- Umepita mwaka mmoja tangu kulipotiwa saini makubaliano baina ya utawala haramu wa Israel na nchi mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain, ambapo mataifa hayo ya Kiarabu yaliafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

Je, makubaliano hayo yameweza kuwa na natija kama zilivyotaraji pande husika zilizotia saini makubaliano hayo?. Maafikiano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain yaliyojulikana kama makubaliano ya Abraham, yalitiwa saini tarehe 15 Septemba mwaka jana (2020) katika ikulu ya Marekani White Housen. Waliohudhuria utiaji saini huo ni Donald Trump aliyekuwa Raius wa Marekani wakati huo, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa zamani wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na  Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain. Miongoni mwa watu wanne waliotia saini makubaliano hayo ya Septemba 15, Netanyahu na Trump kwa sasa hawako madarakani baada ya kubwagwa katika ulingo wa kisiasa. Hii ina maana kwamba, makubaliano hayo hayakuwa na taathira yoyote muhimu hata katika kuwapiga jeki wanasiasa hao na kuwafanya wabakie madarakani.

Hali ya Palestina imekuwa mbaya

Moja ya madai ya watawala wa Imarati na Bahrain yalikuwa kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel kungesaidia kudhamini usalama zaidi kwa Palestina. Hata hivyo baada ya kupita mwaka mmoja tangu kusainiwa makubaliano hayo, imethibitika kuwa, madai hayo hayana ukweli wowote na ni bwabwaja tu kisiasa. Vita vya Seif al-Quds vya Mei mwaka huu ni moja kati ya vielelezo vya wazi vya kuwa kinyume madai hayo kuhusiana na malengo ya makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel. Kwa muktadha huo, makubaliano ya Abraham ya Septemba 20202 siyo tu kwamba, hayajawa na matunda yoyote, bali kivitendo yamepelekea kuongezeka ukandamizaji, utumiaji mabavu na jinai za Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Wapalestina.

Maslahi ya kiuchumi hayajadhaminiwa

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Waisraeli wengi wamefanya safari katika katika nchi mbili za Bahrain na Imarati, balozi za pande mbili huko Manama, Abu Dhabi na Tel Aviv zimefunguliwa, viongozi wa Israel wamefanya safari katika nchi za Bahrain na Imarati kama ambavyo viongozi wa nchi mbili hizo za Kiarabu wamefanya safari huko Tel Aviv. Pamoja na hayo hatua hizo inaonekana kuwa, zaidi zimeweza kuvunjua tu mwiko katika uhusiano wa nchi hizo mbili za Kiarabu na Israel, huku kivitendo zikiwa hazijadhamini maslahi ya kiuchumi ya pande za makubaliano hayo.

Suala jingine linahusiana na maslahi ya makubaliano hayo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Licha ya kuwa, kupitia makubaliano hayo, utawala vamizi wa Israel umeweza kuimarisha uhusiano wake na nchi mbili hizo za Kiarabu na kwa namna fulani kuweza kudhamini maslahi yake ya kisiasa, lakini uhalisia wa mambo ni kuwa, makubaliano hayo hayajaweza kupunguza changamoto za Israel katika nyuga mbili za kiuchumi na kiusalama. Moja ya sababu ya jambo hilo ni kuwa, siyo tu kwamba, hasira na ghadhabu za fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiarabu dhidi ya Israel hazijapungua, bali zinaonekana kushika kasi hasa kutokana na hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo mawili ya Kiarabu kwa upande mmoja, na kushadidi ukandamizaji na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina kwa upande wa pili.

Katika uwanja huo, kituo cha utafiti wa usalama wa ndani cha Israel chenye mfungamano na Chuo Kikuu cha Tel Aviv kimetoa ripoti yake mpya ya kistratijia ambayo imechambua changamoto zinayoyakabili makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida nchi za Kiarabu na Israel. Kituo hicho kimeandika katika ripoti yake hiyo kwamba: Moja ya changamoto kuu katika njia ya makubaliano ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni msimamo wa fikra za waliowengi katika mataifa ya Kiarabu.

Israel haijapata ufumbuzi wa matatizo ya kistratijia

Kama ilivyokuuwa katika makubaliano ya amani na Israel na mataifa ya Misri na Jordan, katika mataifa ya Kiarabu kuna msimamo wa kihafidhina dhidi ya Israel na fikra za waliowengi katika mataifa hayo ni maadui wa makubaliano hayo. Kituo hicho kimesisitiza kuwa, makubaliano haya ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel hadi sasa hayajaweza kuzipatia ufumbuzi changamoto za kistratijia ambazo Israel inakabiliwa nazo.

Gili Cohen, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Runinga rasmi ya Israel akizinukuu duru za ngazi za juu za Tel Aviv anasisitiza kuwa, ilichopata Israel kupitia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida mataifa ya Kiarabu ni kidogo mno kinyume kabisa na ilivyotarajiwa. Baada ya kuwa pande zote za makubaliano hayo kuwa na matumaini makubwa na makubaliano hayo, filihali baada ya kupita mwaka mmoja anga ya fikra za waliowengi imebadilika mno, ingawa mabadiliko haya hayaishii tu katika kubadilika serikali na uongozi nchini Marekani na kuingia madarakani serikali nyingine au baraza la mawaziri huko Israel; lakini ukweli wa mambo ni kuwa, anga jumla katika mataifa ya Kiarabu ina hisia za chuki dhidi ya Israel.

Kwa kuzingatia mazingira haya, mtandao wa habari wa Rai al-Yaoum umeandika katika moja ya ripoti zake kwamba: Mwaka mmoja baada ya kutiwa saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kunaonekana wazi katika ripoti za vyombo vya habari vya Kizayuni suala la kukiri kwamba, makubaliano hayo yameshindwa na kugonga mwamba, na vyombo hivi vya habari vimekuwa vikiakisi hali ya kuchanganyikiwa Israel kuhusiana na matokeo ya makubaliano hayo yaliyopigiwa upatu mno na Donald Trump na Benjamin Netanyahu.

3997991

captcha