IQNA

Chama cha 'Uadilifu na Ustawi' chashindwa vibaya katika uchaguzi Morocco

22:45 - September 09, 2021
Habari ID: 3474275
TEHRAN (IQNA)- Chama katika muungano tawala nchini Morocco kimepata pigo kubwa katika uchaguzi wa Bunge, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afriika.

Kwa mujibu wa matokeo ya muda yaliyotangazwa mapema leo, chama chenye muelekeo wa Kiislamu cha Uadilifu na Ustawi (PJD) kilichokuwa na viti 125 kimepata pigo kubwa na kuambulia 12 tu, kikiwa nyuma sana ya wapinzani wake wakuu, National Rally of Independents (NRI), Authenticity and Modernity Party (PAM), na chama cha Istiqlal (PI). 

Chama kikuu cha upinzani cha NRI kimeshinda viti visivyopungua 97, kwa mujibu wa kura zilizokuwa zimehesabiwa kikifuatiwa na PAM kilichoshika nafasi ya pili kwa kupata viti 82, na PI kikiwa na viti 78.

Kiwango cha ushiriki wa wananchi katika upigaji kura katika uchaguzi wa Bunge wa jana Jumatano kilikuwa zaidi ya asilimia 50, juu zaidi kuliko mwaka 2016.

Morocco ni nchi yenye utawala rasmi wa ufalme wa kikatiba lakini mfalme ana mamlaka makubwa sana. Mfalme wa Morocco anateuwa Waziri Mkuu kutoka chama kinachoshinda viti vingi katika Bunge lenye wawakilishi 395, na vilevile ana mamlaka ya kuteua mawaziri wa wizara muhimu za serikali.

Kasri ya mfalme wa Morocco pia huwa na mamlaka ya kupanga sera za kiuchumi za serikali za nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika yenye jamii ya watu milioni 37.

3996247

Kishikizo: morocco uchaguzi bunge
captcha