IQNA

Wito wa kutuma makala katika Mkutano wa 35 wa Umoja wa Kiislamu

13:37 - September 08, 2021
Habari ID: 3474273
TEHRAN (IQNA)- Waandaaji wa Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu wamealika wasomi, wanafikra na wataalam kutuma makala zao katika kongamano hilo.

Duru ya 35 la Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu itaandaliwa Oktoba kwa njia ya intaneti kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Kongamano hilo litafanyika baina ya Oktoba 24-28 na maudhui kuu katika kongamano la mwaka huu ni ‘Amani na Kuzuia Mifarakano’. Mada  zingine zitakazojadiliwa katika hafla hiyo ya wasomi ni pamoja na "Udugu wa Kiislamu na Kukabiliana na Ugaidi", "huruma na maelewano ya Kiislamu na kuzuia mivutano na mizozo", "kuheshimiana kati ya madhehebu za Kiislamu", "Palestina na upinzani wa Kiislamu" na "kumkumbuka na kumuenzi Ayatollah Mohammad Ali Taskhiri ”.

Wale wanaopenda kushiriki katika mkutano wanaweza kusajili na kuwasilisha makala zao kabla ya Oktoba 4.

Kwa maelezo zaidi kuhusu kutuma makala bonyeza hapa

 

Mkutano huo wa Umoja wa Kiislamu umekuwa ukifanyika kila mwaka tokea mapema muongo wa 80 kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3995465

captcha