IQNA

Hizbullah yapongeza Wapalestina 6 waliotoroka jela ya Israel kishujaa

13:12 - September 07, 2021
Habari ID: 3474270
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imepongeza kitendo cha kishujaa cha Wapalestina sita ambapo walitoroka jela lenye ulinzi mkali la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa, Hizbullah imesema kitendo hicho ni pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni ambap unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu. Hizbullah imesema kitendo hicho cha kutoroka jela yenye ulinzi mkali ni cha kipekee na kuongeza kuwa, “kitendo hicho ni ushahidi wa wazi wa ustadi, subira na mapambano yanayoendelea ya Wapalestina kwa lengo la kukomboa ardhi zao na wafungwa.”

Wakati huo huo, maelfu ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza wameandamana kwa mnasaba wa kusherehekea kutoroka kishujaa mateka sita Wapalestina waliokuwa wakishikiliwa kwenye jela ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mnasaba wa ushindi huo adhimu, wanachama na wafuasi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, Hamas, na wa Harakati ya Jihadul-Islami usiku wa kuamkia leo walifanya maandamano katika mji wa Jabaliya ulioko kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Akizungumza pembeni ya maandamano hayo, msemaji wa Hamas Abdulatif Qanuu amesema, mateka Wapalestina wameweza kuvivuka vigingi vya ulinzi na kiusalama vya adui na kumshinda adui Mzayuni na vyombo vyake vya usalama.

Miji ya Jenin, al Khalil na baadhi ya maeneo mengine ya Ufukwe wa Magharibi, jana yalikuwa uwanja wa maandamano makubwa yaliyofanywa kwa mnasaba wa kuwa huru mateka sita Wapalestina. Washiriki wa maandamano hayo walitangaza mshikamano wao kwa mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala dhalimu wa Kizayuni.

Zakariya Zubeidi (46), Monadel Yacoub Nafe’at (26), Yaqoub Qassem, Yaqoub Mahmoud Qadri (49), Ayham Nayef Kamamji (35) na Mahmoud Abdullah Ardah (46) ni Wapalestina sita ambao wamefanikiwa kutoroka jela yenye ulinzi mkali zaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya Gilboa kupitia mashimo ya chini kwa chini; na hatua za vyombo vya usalama vya utawala huo haramu za kuwakamata mateka hao hadi sasa zimegonga mwamba.

3475645

captcha