IQNA

Umoja wa Mataifa wakosolewa kwa kutojali jinai za Saudia dhidi ya watoto wa Yemen

13:09 - June 24, 2021
Habari ID: 3474038
TEHRAN (IQNA)- Watoto wa Yemen wamelaani vikali uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa muungano vamizi wa Saudia baada ya umoja huo kukataa kukosoa Saudia na waitifaki wake wanaotenda jinai dhidi ya watoto Wayemeni.

Jumanne wiki hii idadi kubwa ya watoto Wayemen waliandamana katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a na kulaani uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kutoiweka Saudia katika orodha ya nchi zinazokiuka haki za watoto.

Wakati huo huo, Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesajili jina lake na taasisi hiyo katika orodha ya fedheha na aibu kwa kuliweka jila la harakati hiyo katika orodha ya makundi yanayokiuka haki za watoto duniani.

Taarifa iliyotolewa na Ansullah imesema kuwa, Guterres amethibitisha kuwa, Umoja wa Mataifa ni jukwaa lisilo na thamani yoyote ambalo linatumiwa na nchi zenye ushawishi mkubwa duniani kwa ajili ya kupotosha ukweli na kukanyaga haki za mataifa yanayokandamizwa. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, ilikuwa vyema UN iwe taasisi isiyopendelea upande wowote na isikariri bwabwaja za muungano vamizi huko Yemen.

Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarullah nchini Yemen imesema kuwa, hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kuliweka jina la harakati hiyo katika orodha ya wakiukaji wakubwa wa haki za watoto haikutegemea ushahidi wa aina yoyote wa maana na kwamba kwa hatua hiyo, Umoja wa Mataifa umekata uhusiano wake na taifa la Yemen na kujiunga na muungano wa nchi zilizoivamia nchi hiyo.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Taasisi moja ya kutetea haki za binadamu nchini Yemen ilitangaza mwezi Oktoba mwaka jana kuwa kuwa wanawake na watoto zaidi ya elfu 13 wa Kiyemeni wameuawa katika mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini humo.

Taasisi ya Haki za Binadamu ya Insaf ambayo inatetea haki za watoto na wanawake wa Yemen  ilitoa ripoti na kueleza kuwa, idadi sahihi ya wanawake na watoto wa Yemen waliouliwa na kujeruhiwa hadi kufikia Ijumaa ya tarehe 9 Oktoba mwaka huu ni elfu 13 na 73.  

Taasisi hiyo ya haki za binadamu imeeleza kuwa, wanawake 5,183 na watoto 7,891 wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake tangu muungano huo uanzishe hujuma zake katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Ripoti ya taasisi ya haki za binadamu ya Insaf imeongeza kuwa, mamia ya vituo vya afya vya wanawake na watoto pia vinakaribia kufungwa baada ya muungano vamizi wa Saudia kuzuia kuingizwa nishati nchini Yemen na kwamba suala hilo litasababisha maafa makubwa ya kibinadamu. 

Katika ripoti hiyo, taasisi ya haki za binadamu ya Insaf imeeleza kuwa, mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taasisi  za elimu za Yemen pia yamewaathiri karibu wanafunzi milioni mbili. Taasisi  hiyo imetaka kufanyike uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu jinai zilizofanywa na muungano vamizi wa Saudia na kuhukumiwa wahusika wa jinai hizo. 

Hivi karibuni pia  Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen aliweka wazi athari mbaya za mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen na kuzingirwa nchi hiyo ya Kiarabu.

3475028/

Kishikizo: watoto yemen
captcha