IQNA

Malaysia yalenga kuwa nchi ya Kiislamu yenye kufuata Qur’ani, Hadithi

23:56 - August 02, 2018
Habari ID: 3471616
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Muhammad amesema nchi yake ina azma ya kuwa taifa la Kiislamu lenye kufuata mafundisho ya Qur’ani na Hadithi sahihi.

Akizungumza wiki hii katika mkutano maalumu wa maulamaa na wasomi Waislamu ofisini kwake mjini Putrajaya,  Mahathir amesema serikali yake inalenga kuifanya Malaysia iwe mfano wa kuigwa wa taifa bora zaidi la Kiislamu katika dunia ya sasa. Aidha amebainisha masikitiko yake kuwa ulimwengu kwa kawaida huunisibisha Uislamu na vita, ghasi na udhaifu wa kiuchumi. Mahathir ametoa wito kwa maulamaa na wasomi Waislamu kutumia fursa iliyojitokeza katika serikali yake kueneza fikra za Uislamu sahihi na wenye rehema. Katika kikao hicho, waziri mkuu wa Malaysia aidha alijadili mbinu kadhaa za kuzipa nguvu taasisi za Kiislamu ili zisijikete tu katika masuala ya ibada za kila siku bali pia zishughulikie masuala ya sayansi na uchumi.

Mahathir pia ametaka kuwepo mikakati maalumu ya kikabiliana na wale wenye misimamo ya kufurutu ada wasa wale wenye itikadi potovu za kuwakufurisha Waislamu wenzao.

Mwezi Mei, Mahathir, alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo na kutangazwa kuwa waziri mkuu. Dakta Mahathir Mohamad mwenye umri wa miaka 93, alitoka katika maisha ya kustaafu na kuja kuiongoza tena Malaysia, baada ya nchi hiyo hiyo kukabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na mfumkoa wa bei za bidhaa muhimu.

Mahathir aliwahi kuwa waziri mkuu wa Malaysia mwaka 1981 hadi 2003 wakati nchi hiyo iliposhuhudia ustawi mkubwa na maisha bora jambo ambalo limewafanya Wamalaysia kumchagua tena wakitumai kurejea tena zama zake za maendeleo ya kasi na yenye manufaa kwa wananchi wote. Waislamu Malaysia wanakadiriwa kuwa milioni 19.5 au asilimia 61 ya watu wote wan chi hiyo ya kusini magharibi mwa Asia.

3466458

captcha