IQNA

Uganda yaidhinisha sheria za mfumo wa benki za Kiislamu

17:02 - February 05, 2018
Habari ID: 3471381
TEHRAN (IQNA)-Serikali ya Uganda imeidhinisha sheria za mfumo wa benki za Kiislamu huku benki kuu nchini humo ikitazamiwa kuchapisha rasmi sheria hizo kama sehemu ya mikakati ya kuwashirikisha Waislamu kikamilifu katika mfumo wa kifedha.

Baada ya sheria hizo kuchapishwa rasmi, Benki Kuu ya Uganda itapokea maombi ya taasisi za kifedha ambazo zinalenga kutoa huduma zinazoenda sambamba na mafundisho ya Kiislamu, amesema gavana wa benki hiyo Emmanuel Tumusiime-Mutebile wakati akihutubu katika Jumuiya ya Benki za Binadamu.

Uganda inajiunga nchi jirani za Kenya, Tanzania na Ethiopia ambazo tayari zimeruhusu benki na taasisi za kifedha kutoa huduma za Kiislamu pasina kutoza riba nk.

Mfumo wa kifedha wa Kiislamu kimsingi huendeshwa kwa msingi wa mafundisho ya dini hiyo tukufu ambayo imeharamisha riba.

Mwezi Disemba, Benki Kuu ya Uganda ilijiunga na kuwa mwanachama wa Baraza la Bodi ya Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFSB) ambayo ina makao yake huko Kuala Lumpur Malaysia. IFSB NI bodi ya kimataifa inayoweka viwango na kustawisha huduma za kifedha za Kiislamu zenye uwazi na usimamizi bora duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya IFSB yam waka 2016, sekta ya huduma za kifedha za Kiislamu ilikuwa na thamani ya $ trilioni 1.88 mwaka 2015.

3688845

captcha